Na. Dennis Gondwe, Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Watendaji wa Wilaya ya Kilolo wametakiwa kukusanya na kusimamia mapato ya Serikali ili kuongeza wigo wa Serikali kuhudumia wananchi wake.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akiongea watendaji wa Wilaya ya Kilolo katika majumuisho ya ziara yake ya Tarafa kwa Tarafa wilayani Kilolo jana.
Mhe Hapi alisema kuwa mapato ya Serikali ni jambo la msingi kwa uendeshaji wa shughuli za Serikali.”Msiwe na mzaha kwenye kukusanya mapato ya Serikali. Mapato ya serikali ndiyo yanayotumika kugharamia miradi ya maendeleo” alisisitiza Mhe Hapi. Vilevile, aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo wa mapato yake. “Ndugu zangu, ukusanyaji mapato uende sambamba na usimamizi wa mapato hayo ili yatumike kwa kazi iliyokusudiwa” alisema Mhe Hapi.
Aidha, alisisitiza usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Kilolo. Alitoa pongezi kwa ujenzi wa hospitali ya wilaya unaoendelea na miradi mingine ya maendeleo. Aidha, aliwaagiza Wakala wa ujenzi nchini (TBA) kumsimamia vizuri mkandarasi anayejenga hospitali hiyo ili ajenge kwa viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa matakwa ya mkataba.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amemaliza ziara yake siku siku tatu kutembelea Tarafa tatu za Wilaya ya Kilolo na kuanza ziara ya kutembelea Tafara za Wilaya ya Iringa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.