Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Watalaam wa sekta ya elimu wilayani Kilolo wametakiwa kuielimisha na kuihamasisha jamii kuunga mkono juhudi zinazofanywa za kujenga miundombinu ya elimu kwa lengo la kukuza utoaji wa huduma hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa maendeleo ya sekta ya elimu wilaya ya Kilolo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Kilolo.
Masenza alisema kuwa shule wilayani Kilolo zinachangamoto ya miundombinu, utoaji wa chakula cha mchana na usimamizi makini wa utekelezaji wa sera ya elimu. “Sote kwa pamoja tunawajibika kuihamasisha jamii juu ya kuchangia maendeleo ya taasisi zetu za kielimu. Jukumu la kuhakikisha shule zetu zina miundombinu madhubuti ni la jamii inayotuzunguka kwa ubia na serikali yetu ya awamu ya tano. Wajibu wetu ni kuielimisha jamii juu ya hili na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na jamii” alisema Masenza. Yapo maeneo ambayo yamefikia mafanikio makubwa, ambayo yanatakiwa mafanikio hayo kuambukizwa maeneo ambayo hayafanyi vizuri, aliongeza.
Mkuu wa Mkoa aliwataka wadau wa maendeleo ya sekta ya elimu wilaya ya Kilolo kuchambua na kushirikishana mipango itakayoleta maendeleo thabiti katika sekta ya elimu. Aidha, aliwataka kujenga ari ya ushindani na kupigania nafasi za ushindani wa juu zaidi katika kufikia mafanikio ya sekta ya elimu. Aliwataka kutumia kikao hicho kuongeza juhudi na ubunifu utakaosaidia kutatua changamoto na kuongeza ufanisi katika kuendeleza sekta ya elimu.
Kikao cha wadau wa sekta ya elimu Wilaya ya Kilolo kinalenga kuwakumbusha wajibu katika kufikia mafanikio ya sekta ya elimu pamoja na kushirikishana changamoto na kujadili suluhisho la pamoja.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.