Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi amekataa kuweka jiwe la msingi jengo la kliniki ya uzazi na afya ya mtoto katika kituo cha afya Mgololo, wilayani Mufindi baada ya kutoridhishwa na gharama kubwa za ujenzi zilizotumika.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya Tarafa kwa Tarafa ya kutembelea Tarafa 15 za Mkoa wa Iringa, iliyoanzia katika Tarafa ya Kasanga Wilaya ya Mufindi, alipangiwa kutembelea na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la kliniki ya uzazi na afya ya mtoto. Mhe Hapi alikataa kuweka jiwe la msingi baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo lililogharimu kiasi cha shilingi milioni 360. “Siwezi kuweka jiwe la msingi katika jengo hili. Nataka kujiridhisha na thamani ya fedha katika mradi huu. Mnapotengeneza makadirio ya gharama za ujenzi wa mradi (BOQ) makubwa mnamkatisha tamaa muwekezaji. Nataka maelezo kutoka Wakala wa ujenzi Tanzania (TBA) nani kaandaa makadirio ya gharama za ujenzi wa mradi huu” alihoji Mhe Hapi. Maeneo mengi tumejenga Zahanati kwa gharama za shilingi milioni 400, iweje jengo hili tu la kliniki ya uzazi na afya ya mtoto ligharimu shilingi milioni 360, aliendelea kuhoji, Mhe Hapi.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo la kliniki ya uzazi na afya ya mtoto, katika kituo cha afya Mgololo kwa Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt Fredrick Mugarula alisema kuwa ili kukamilisha ujenzi wa jengo la kliniki hiyo, imekadiriwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 360. “Serikali kupitia ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa na TBA wameweza kutoa marekebisho ya ramani na makisio ya ujenzi” alisema Dkt Mugarula.
Akiongelea matarajio ya mradi huo, alisema kuwa baada ya ujenzi kukamilika, Halmashauri inatarajia kuwa na ongezeko kubwa la wateja katika kliniki hiyo kutokana na mazingira yenye kutoa huduma bora. Aidha, hali hiyo itapunguza vifo vya kina mama na watoto vilivyokuwa na uhusiano wa kutopata huduma bora za afya.
Kituo cha afya Mgololo ni miongoni mwa vituo tisa vya afya vinavyotoa huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, kikiwa kilianzishwa mwaka 1985 na Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere kama sehemu ya kiwanda cha karatasi Mgololo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.