Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Hofu ya matukio ya vifo imesababisha watu wengi kutosajili matukio hayo yanapotokea na kupekelea asilimia 17.5 ya usajili nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha hamasa kwa viongozi wa Mkoa wa Iringa kuhusu majaribio ya mpango wa usajili wa vifo, kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Masenza alisema kuwa wananchi wamekuwa wakiogopa matukio yanayoambatana na kifo. Woga uliopo ndio unasababisha wananchi wengi kutosajili matukio ya vifo yanapotokea. Woga huyo umesababisha nchi kuwa na wastani wa asilimia 17.5 ya vifo vilivyotokea na kusajiliwa. “Ni imani yangu kwamba tunaenda kubadili hali hii na kama ilivyokuwa kwa usajili wa watoto wadogo ambapo tulikuwa asilimia 11.7 na ndani ya miezi mitatu tukaweza kufika asilimia 100, hivyo naamini tutafanikisha zoezi hili kwa kasi hiyohiyo” alisema Masenza.
Jamii inatakiwa kuhamasishwa kubadili tabia na kuona umuhimu wa kusajili kila tukio la kifo linapotokea. “Wananchi wengi ambao hawana matumizi ya moja kwa moja na cheti cha kifo cha ndugu zao wamekuwa hawafiki RITA kusajili na changamoto kubwa hapa naiona ni kukosa uelewa wa umuhimu wake hivyo kushindwa kubadili tabia” alisema. Ni vigumu kwa mwananchi kuona uhusiano kati ya yeye kusajili kifo cha ndugu yake na maendeleo ya nchi alisema. “Nafahamu zipo nchi ambazo walishaacha kufanya sensa kama tunayofanya kila baada ya miaka kumi na kutumia fedha nyingi kwani nchi hizo wameweka utaratibu ambapo kila mtoto anayezaliwa anasajiliwa na kila mtu anayefariki anasajiliwa hivyo wanakuwa na takwimu za wananchi wake kila siku” alisema Masenza.
Katika kufanikisha zoezi hili, uhamasishaji wa hali ya juu unahitajika alisema mkuu wa Mkoa. Aidha, aliwataka wajumbe wote kuhakikisha ujumbe sahihi unawafikia wananchi ambao wanahitajika kubadili fikra na kuanza kuwa na mtazamo chanya katika usajili wa matukio ya vifo, alisema.
Majaribio ya maboresho ya mfumo wa usajili wa vifo yanafanyika kwa mara ya kwanza katika Mkoa wa Iringa kutokana na mkoa huo kufanya vizuri katika zoezi la usajili watoto wenye umri chini ya miaka mitano na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.