Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Watumishi 235 wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa wamepatiwa mafunzo ya kupambana na rushwa mahala pa kazi ili waweze kuwahudumia wananchi vizuri.
Akisoma risala ya utii ya wananchi wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa Rais Dkt John Magufuli katika uwanja wa mkesha wa Mwenge wa uhuru, Isimani Tarafani, kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Iringa, Mariam Mlilapi alisema kuwa halmashauri kwa kushirikiana na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wametoa mafunzo ya kupambana na rushwa kwa watumishi. “Katika kipindi cha Januari- Mei, 2018 halmashauri imefanikiwa kutoa mafunzo ya kupambana na rushwa mahala pa kazi kwa watumishi 235 wa makao makuu ya halmashauri. Mafunzo hayo yalitolewa kwa kushirikiana na maafisa kutoka TAKUKURU” alisema Mlilapi. Lengo la mafunzo hayo kwa watumishi ni kuwataka kuwa waadilifu na kutoa huduma bora kwa wananchi, aliongeza.
Akiongelea hamasa ya kupambana na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa, kaimu Katibu Tawala huyo alisema kuwa halmashauri hiyo imehamasisha na kuanzisha klabu za kupinga rushwa shuleni. Klabu hizo zimeanzishwa katika shule 10 za sekondari zenye jumla ya wanaklabu 300 na shule za msingi 50 zenye jumla ya wanaklabu 1,500 alisema.
Ikumbukwe kuwa halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina wakazi 254,032 kwa mujibu wa sense ya mwaka 2012 wanaume wakiwa 123,243 na wanawake 130,789, ikiwa na Tarafa sita, Kata 28 Vijiji 133, Vitongoji 747 na Kaya 60,160.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.