Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali inajivunia mchango wa wanawake katika kuleta maendeleo ya familia na taifa kutokana na sera nzuri zilizowekwa nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo makandarasi wamawake katika ushiriki kwenye kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara katika ukumbi wa chuo cha VETA mjini Iringa.
“Ni jambo la kujivunia kuwa wanawake wa nyanda za juu kusini
mnajitoa na kuthubutu kwa kadiri muwezavyo kuleta maendeleo
yenu na taifa letu kwa jumla. Napenda kuwahakikishia kuwa ni sera
ya Serikali yetu kuwahamasisha wanawake kushiriki katika kazi za
ujenzi wa barabara” alisema Masenza. Aidha, aliwashauri
wanawake kuchangamkia fursa za miradi ya barabara ili
kuwaongezea mapato. Kwa kufanya hivyo ustawi na kipato kwa
familia zenu na jamii kwa ujumla utaongezeka na hatimaye
kutokomeza umaskini, aliongeza.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo katika maeneo ya uongozi kama wamiliki wa kampuni kwa kuwapa uwezo wa kuongoza wafanyakazi na vibarua. Aidha, alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutunza hesabu na fedha ili kutambua faida na hasara mapema.
Mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo makandarasi wanawake yalihudhuriwa na washiriki kutoka mikoa ya Iringa, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi. Aidha, yalilenga kuwajengea uwezo na uthubutu makandarasi wanawake kushiriki katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.