Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Jamii imetakiwa kujenga utamaduni wa uadilifu katika kuitikia sheria ya maadili ya viongozi wa umma na kanuni za serikali za mitaa nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua semina kwa waheshimiwa madiwani na wakuu wa idara na vitengo wanawake katika Mkoa wa Iringa kuhusu maadili ya viongozi wa umma katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Masenza alisema kuwa uadilifu sharti ujengwe ndani ya jamii ili kuwa utamaduni wa nchi. “Sheria ya maadili ya viongozi wa umma, kanuni za serikali za mitaa pamoja na vyombo vya kusimamia utawala bora pekee haviwezi kufanikisha suala la kukuza na kusimamia maadili. Jukumu la kukuza na kusimamia maadili ya viongozi wa umma linahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya viongozi, wananchi na wadau mbalimbali” alisema Masenza.
Viongozi wanawake wana dhamana na ushawishi mkubwa katika jamii, hivyo wanapashwa kuongoza katika juhudi za kukuza maadili kwa vitendo. “Hatuna budi kuwahamasisha wananchi kuchukia vitendo vya ukiukwaji maadili na kuwakataa viongozi wasio waadilifu. Ni matumaini yangu kuwa elimu mtakayoipata katika semina hii mtaitoa pia kwa wanawake wengine katika Halmashauri zenu, wananchi katika Kata zenu na, Mitaa ambako mnatekeleza majukumu yenu ya kila siku” alisema Masenza.
Moja ya misingi ya demokrasia ni kuwa na Serikali inayowajibika kwa wananchi na yenye viongozi wanaowatumikia wananchi kwa uadilifu, alisema. Wananchi wanategemea viongozi watatumia nafasi zao za uongozi kuwaletea maendeleo na sio vinginevyo, aliongeza. “Sote tunafahamu kwamba uongozi ni dhamana. Kiongozi yeyote, awe ni wa kuchaguliwa ama wa kuteuliwa, amekabidhiwa madaraka na wananchi” alisema. Viongozi wa kisiasa na watumishi wa umma wanatakiwa kutumia nyadhifa zao kwa manufaa ya wananchi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.