Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wananchi mkoani Iringa wametakiwa kushiriki kikamilifu katika uzinduzi wa kampeni ya furaha nyangu ya kupima virus vya ukimwi na kuanza dawa mapema za kufubaza virus vya ukimwi.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, amina masenza alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu ya kupima virus vya ukimwi na kuanza tiba mapema katika ofisi ya mkuu wa mkoa jana.
Masenza alisema kuwa ni muhimu kwa wananchi wote kujitokeza kushiriki katika uzinduzi wa kampeni hiyo. “Nitoe wito kwa Wananchi wote kushiriki kikamilifu katika uzinduzi na mwitikio wa Kampeni hii muhimu kwa mkoa wetu. Baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo, huduma zitaendelea kutolewa katika hospitali zote, vituo vyote vya afya na Zahanati zote mkoani Iringa” alisema masenza.
Kampeni hii ya Kupima na kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU mapema inakwenda na kaulimbiu ya ujumla isemayo “Furaha Yangu” – Pima, Jitambue, Ishi inaanza kwa kuwalenga Wanaume na kisha makundi mengine ya watu walio katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi ya VVU, aliongeza. Aliyataja makundi hatarishi kuwa ni wasichana walio katika umri wa balehe, wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24, akinamama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa uzinduzi wa kampeni ya “Furaha Yangu” unaonesha dhamira ya serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha kuwa kasi ya mapambano ya VVU na UKIMWI, inaongezwa ili kufikia zile “tisini tatu” ifikapo mwaka 2020. Alizitaja kuwa ni asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali zao za maambukizo; asilimia 90 ya waliopimwa VVU na kugundulika kuwa wana maambukizo wapatiwe dawa za kufubazamakali ya VVU; na asilimia 90 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU.
Kampeni ya “Furaha Yangu” itazinduliwa katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa tarehe 24 Julai, 2018 kuanzia saa mbili asubuhi na kuendelea kwa kipindi cha miezi sita ikitarajiwa kuwafikia na kuwapima watu 90,000.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.