Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka
RAS awapongeza wafanyakazi wake
Wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wamepongezwa kwa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na moyo wa kujituma kwa mwaka wa 2009/2010.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka katika kikao kilichofanyika baina yake na wafanyakazi hao, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa leo tarehe 1 Februari, 2010.
Akitoa pongezi hizo, Bibi. Mpaka alisema “nawapongeza wafanyakazi wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa toka moyoni mwangu kwa kazi nzuri, ufanisi na moyo wa kujituma kwa mwaka tuliomaliza wa 2009”.
Akifafanua mizizi ya pongezi hizo Bibi. Mpaka alisema “taarifa za mkoa wa Iringa tunazozipeleka katika ngazi ya Taifa zinapongezwa sana kutokana na ustadi na uchapakazi wa wafanyakazi wa ofisi hii”.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alisisitiza umuhimu wa elimu na maadili kwa wafanyakazi wa umma, alisema “tuna bahati ya kuwa na vyuo vikuu kadhaa Mkoani hapa kama chuo kikuu Huria Tanzania, chuo kikuu cha Tumaini, chuo kikuu cha Mkwawa na chuo kikuu cha Ruaha hivyo tutumie nafasi hii kwa umakini mkubwa kuweza kujipatia elimu zaidi”. Aidha ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa imeandaa mpango wa mafunzo ambao wafanyakazi wamekuwa wakipelekwa katika mafunzo malimbali. Katibu Tawala Mkoa amesema “fedha za mafunzo si nyingi ila tumeanza na kunautaratibu angalau kila mfanyakazi aweze kupata mafunzo hayo”. …(Wafanyakazi wangapi wamepelekwa shule na mafunzo?) .. ..
Wakati huohuo Bibi. Mpaka alichukua nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa michezo kwa afya ya wafanyakazi wa umma. Bibi. Mpaka amesisitiza kuwa “tushiriki wote michezo kwa afya zetu”. Alitoa changamoto kwa timu ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa itakayoshiriki katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka 2010 jinsi itakavyochanua na kurudi na medali na vikombe kadhaa. Katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika mkoani Morogoro mwaka jana, timu hiyo maarufu kama timu ya RAS ilimaliza mashindano hayo na kurejea mikono mitupu bila hata kupata ushindi wa timu yenye nidhamu. Katibu Tawala Mkoa alihoji tabia inayokomaa ya wanamichezo kutokujiandaa kwa mashindandano kwa muda muafaka na badalayake kusubiri mpaka muda wa majeruhi, akisema tabia hii ndiyo inayochangia matokeo mabovu.
Bibi. Mpaka ambaye pia ni bingwa wa mchezo Pete katika miaka ya 1970s alitoa kibwagizo kwamba kutokana na wingi wa shughuli zake itabidi Daktari amuandikie ‘dozi ya michezo’.
Akizungumzia janga la UKIMWI aliwataka wale wote waliogundulika kuwa na VVU kufika ofisini kwake na ili kuweza kupatiwa chakula cha msaada. Katika hospitali ya Mkoa wa Iringa wafanyakazi 15 wamejitokeza kuwa na VVU na kuweza kupatiwa msaada wa chakula.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wafanyakazi wote Bwana. Barnabas Ndunguru alimshukuru Katibu Tawala Mkoa kwa kukutana na kuzungumza na wafanyakazi wote. Aidha Bwana. Ndunguru ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu alitumia fursa hiyo kuhakikisha kuzifanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza ili kuleta ufanisi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
|
Iringa tunzeni vyanzo vya maji
Wananchi wa Mkoa wa Iringa wamekumbushwa kutunza vyanzo vya maji kwa manufaa ya uhai wa vizazi vijavyo.
Ukumbusho huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa. Mohamed Abdulaziz wakati wa uzinduzi wa wiki ya upandaji miti kimkoa uliofanyika katika Kata ya Wanyama, Tarafa ya Imalinyi, Wilaya ya Njombe tarehe 10 Januari, 2010.
Katika hotuba yake Mheshimiwa. Abdulaziz alisisitiza “tutunze vyanzo vya maji kwani maji ni uhai wetu”. Aliongeza kwa kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika tuzo ya Mheshimiwa. Rais Jakaya Kikwete inayohusu upandaji miti, utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira ili Mkoa wa Iringa uwe mfano kitaifa.
Mkuu huyo wa Mkoa amekemea tabia inayoendelea kukua baina ya wananchi wa Iringa ya kulima na kulisha mifugo katika vyanzo vya maji.
“…tuache kulima karibu na vyanzo vya maji, kufyatua matofali na kulisha mifugo na kuharibu mazingira”.
Aidha aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na wataalamu katika kuhakikisha kuwa vyanzo vyote vya maji vinatunzwa na kuhifadhiwa.
Mheshimiwa. Abdulaziz alisisitiza kuwa pamoja na umuhimu wa kupanda miti, muhimu zaidi ni kutunza miti hiyo iliyopandwa na kuilinda kwa nguvu zote dhidi ya moto na mifugo inayochungwa katika maeneo yaliyopandwa miti.
Mkuu wa Mkoa aliagiza ifanyike sensa ya miti ili Mkoa uwe na takwimu sahihi zinazoonesha idadi ya miti iliyopo mashambani mwaka mmoja baada ya upandaji.
Mkuu wa Mkoa alizishukuru na kuzipongeza Halmashauri zote zinazotenga fedha za kuanzisha misitu ya kupandwa, na kuzitaka Halmashauri hizo ziwe na mashamba ya miti ya mfano yanayotunzwa vizuri ili wananchi wajifunze utaalamu wa upandaji miti na utunzaji wake.
Katika kipindi cha Januari 2001 hadi Januari 2009, Mkoa wa Iringa ulipanda zaidi ya miti milioni 5,603,296.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa. Mohamed Abdulaziz akipanda mti wa kumbukumbu katika wiki ya maadhimisho ya upandaji miti kimkoa Wilaya ya Njombe .

Baadhi ya wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakimsikiliza Katibu Tawala Mkoa.
|